Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, sambamba na kuongezeka kwa joto la ushindani wa uchaguzi nchini Chile, jamii ya Wapalestina nchini humo, imetuma ujumbe wa wazi kwa wagombea wa urais. Maurice Khamis, rais wa jamii ya Wapalestina wa Chile, katika hafla ya kila mwaka iliyopewa jina “Kutoka Bethlehemu hadi Chile: Mwanga wa Tumaini,” alisisitiza kuwa sera ya mambo ya nje ya Chile kuhusu Palestina si msimamo wa muda mfupi, bali ni nguzo ya kudumu ya utambulisho wa kidiplomasia wa nchi hii, na inapaswa kuendelea kujengwa juu ya misingi, maadili na heshima ya haki za mataifa.
Khamis, akibainisha kuwa “katika wiki chache zijazo, Chile itamchagua rais mpya,” alionya kuwa mabadiliko ya serikali hayapaswi kupelekea mabadiliko ya msimamo wa nchi hii kuhusu suala la Palestina. Alisema: “Tunatarajia kutoka kwa yeyote atakayeshika hatamu za uongozi baada ya uchaguzi, alinde msimamo wa heshima na thabiti wa Chile kuhusu Palestina; msimamo unaojengwa juu ya uadilifu, utu wa binadamu na utetezi wa sheria za kimataifa ambao umeipatia nchi heshima ya kidiplomasia kwa miongo kadhaa.”
Aliongeza kuwa katika mazingira ambayo ulimwengu umejaa migogoro na kutokuwa na utulivu, ni muhimu kwa Chile kuendelea kufuata mwelekeo wake huo huo ulio wazi: “Katika nyakati kama hizi, kujitolea kwa misingi kuna umuhimu mkubwa zaidi kuliko wakati mwengune wowote ule—misngi ambayo imeifanya nchi yetu iwe tofauti katika uwanja wa kimataifa; misingi kama utetezi wa haki za binadamu, heshima kamili kwa sheria za kimataifa, na upinzani usio na shaka dhidi ya aina yoyote ya uhalifu wa kivita.”
Maurice Khamis aliendelea kwa kulitaka pia Bunge jipya lililochaguliwa kuimarisha ahadi ya muda mrefu ya Chile kwa haki za kimataifa. Alisema: Bunge jipya, ambalo ni kielelezo cha matakwa ya wananchi, lina nafasi muhimu katika kuilinda njia hii ya kihistoria. Tunawaomba wabunge wapya wasiendeleze tu msimamo huu ulio wazi, bali wauthibitishe zaidi, ili uungwaji mkono wa Chile kwa haki ya kujitawala ya taifa la Palestina na haki za binadamu uonekane kwa uwazi zaidi kuliko hapo awali.
Kwa mujibu wa wachambuzi, kauli hizi zilitolewa katika wakati nyeti ambapo sera ya mambo ya nje ni miongoni mwa mada zinazojadiliwa kwa joto kubwa katika mijadala ya uchaguzi wa Chile, na jamii ya Wapalestina wa nchi hiyo inajitahidi kuifanya sauti yake iwe na athari katika mijadala hiyo.
Maoni yako